Saturday, May 27, 2017

Namna muziki wa G Nako ulivyojigawa

G NAKO ni msanii ambaye sauti yake ni bidhaa ambayo inauzika kirahisi katika soko la muziki wa bongo fleva kwa sasa.
Rapa huyu ameweza kuhakikisha unauza bidhaa yake vema tangu kipindi cha Nako 2 Nako Soldiers, hadi kipindi hiki cha Weusi.
Ingawa inafahamika chimbuko lake ni katika muziki wa hip hop, ila amekuwa hatabiriki katika aina yake ya muziki anaofanya.
Amekuwa anabadilika kila mara, lakini cha ajabu bado anasalia na mashabiki wake wale wale.
Leo katika zeze kolabo napenda kukuchambulia jinsi G Nako alivyoshirikishwa na wasanii wa kuimba na wale wa kurap (hip hop).
 
Ngumu nyeusi
Wasanii wengi wa hip hop wanapomshirikisha G Nako hupenda aimbe kiitikio (chorus) katika nyimbo zao na si kurap.
Hufanya hivi ili kuleta utofauti kwani kinachotakiwa ni ile sauti yake yenye kuamsha ‘mizuka’. Wasanii hawa walifakiwa kufanya hivyo.
Izzo Business na Mwana FA
Tukianza na Izzo Business, mwaka jana alimshrikisha G Nako katika wimbo wake uitwao ‘Shem Lake’ ambao alikuwepo na Mwana FA pia. Wimbo huu ilifanyika studio za The Industry kwa prodyuza Nahreel.
Kabla ya hii ngoma, Mwana FA alikuwa ameshafanya wimbo na G Nako uliofamika kama ‘Mfalme’ kutoka kwenye mikono ya prodyuza Marco Chali wa MJ Recods.
 
Stereo na Country Boy
Hawa ni marapa ambao tunaweza kuuweka muziki wao sehemu moja katika kiwango cha ushindani, kama wanazidiana si kwa kiwango kikubwa.
Stereo ambaye anawakilisha Tamadunimuziki alimpa shavu G Nako kwenye wimbo uliokwenda kwa jina la ‘Sana’ chini prodyuza Rash Don wa Kiri Records.
Kwa upande wa Country Boy ameshafanya kazi mbili na G Nako, hii inamaanisha kufanya kazi na G Nako ni biashara nzuri na inayolipa.
Wimbo wa kwanza ulifamika kama ‘Watch me’ uliotoka mwaka 2013, kisha kufutiwa na wimbo uitwao ‘Mtaa kwa mtaa’. Hizi zote nilishawahi kuzichambua katika kolamu hii siku za nyuma.
Laini pia zipo
Pia wasanii wa kuimba katika miondoko tofauti tofauti kama zuku na Rnb nao hawakuwa mbali kuinasa sauti ya G Nako.
Hawa walimtafuta G Nako ili aje kurapa katika nyimbo zao, lakini lile kundi la kwanza (hip hop) ilikuwa ni kinyume na hao.
Hapa ndio inakuja maana kamili ya ‘G Nako wa ngumu na laini’. Wafuatao walifanikiwa kufanya hivyo.
 
Rama Dee na Damian Soul
Hawa wote wanafanya muziki unaoshabiana kwa kiasi kikuwa, Rama Dee akifanya Rnb, hivyo kwa Damian Saul ila amekuwa akibadilika mara kwa mara.
Alimpa shavu G Nako kwenye wimbo uliofahamika kama ‘Make up’ iliotoka mwaka 2011 chini ya prodyuza Pancho Latino wa B Hit’s.
Kwa upande wa Damian Saul alimpa shavu G Nako katika wimbo wake uitwao ‘Tudumishe’ uliotoka mwaka jana chini ya studio za Legendary Music.
Mwisho ni wimbo wa ‘Chizika remix’ wa kundi la Fly But Ghetto (FBG) kutoka Arusha ambapo na DJ Fetty alipewa shavu katika wimbo huo.
Pia G Nako ameimba na kurap kwenye nyimbo kama ‘Show love’ ya Nako 2 Nako Soldiers, ‘Bum Kubum’ ya Nikki wa Pili na ‘Gere’ ya Weusi.
 
Wenyewe athibitisha
Niliyoandika hapo juu yanathibitishwa na yeye wenye kwa kuangalia namna anavyokuwa akifanya katika nyimbo zake binafsi.
Kuna baadhi ya nyimbo zake amewashirikisha wasanii wanaoimba, na nyingine wanaorap (hip hop), tuaze kwa wanaoimba, ni kama ifutavyo.
 
Peter Msechu, Ben Paul na Baby J
Tukiaza na Peter Msechu, G Nako alimshirikisha kwenye wimbo uitwa ‘Bado ngware’, ambao ‘remix’ yake alimshirikisha Nikki wa Pili.
Ben Paul alisikika katika wimbo wa ‘Mama Yeyo’ ulitoka mwaka 2013 chini ya maprodyuza Mona Gangsta na Chizan Brain.
Na mwisho ni Baby J kutoka Zanzibar   ambaye alipewa shavu katika wimbo uitwa ‘Oh oh’.
Funga Kazi
Tunamaliza na wale wasanii wa hip hop ambao G Nako amewashirikisha kwenye nyimbo zake.
Godzilla alipewa shavu katika wimbo uitwao ‘Tumewaka’ ulitoka mwaka 2014.
Pia wakali Chindo Man na JCB walishirikishwa kwenye wimbo ulitwao ‘Bado muda kidogo’ chini ya prodyuza DX. Katika nyimbo hizi mbili G Nako ameimba na kurap pia.
 

Na Peter Akaro
Kwa maoni 0755 299 596

0 Comments: