Saturday, May 27, 2017

Vyovyote itakavyokuwa muache Lulu awe hapo alipo


UMEWAHI kumsikia mtu anaitwa Mauclay Culkin? Eeh inawezekana hilo jina likawa gumu masikioni mwako, hata ukinambia kuwa hujawahi kumsikia wala sitokushangaa. Twende taratibu tutafika.
Vipi kama nitakutajia Kevin McCallister? Hapa najua wote tutajenga tabasamu kwa maana tunamfahamu, kutokana na ubora wake aliouonesha kwenye movie ya Home Alone ambayo iliingiza zaidi ya Dola Milioni 400 ya mauzo yake.
Mauclay Culkin ndie Kevin wa Home Alone akiwa na miaka 10 alikuwa staa mkubwa Marekani na Dunia kwa ujumla, aliwateka watu kuanzia sura yake ya kitoto hadi ubora wake ndani ya movie ile. Weka pini hapo.
Katika umri mdogo, sura ya kitoto na hata uzito mdogo wa sauti bado havikuzuia Dunia kumjua Shad Mos a.k.a Lil Bow Bow Rapa ambaye aliuteka Ulimwengu katika umri wa miaka 13.
Kolabo yake ya that’s my Name na Mkali Snoop Dogg ikazidi kumueka katika chati mbalimbali za Runinga na vituo vya Radio, akafanikiwa kupata fedha nyingi huku wengi wakijaribu kumfananisha na Rapa mwenzake Lil Wayne.
Elizabeth Michael ‘Lulu’ ni mmoja kati ya wasanii wa kike ambao walitoka wakiwa na umri mdogo, akiwa na kundi la Kaole alifanikiwa kutengeneza jina lake kwa kasi kubwa huku mashabiki wa zile Tamthilia zilizokuwa zikiruka kila siku ya Jumamosi saa 2:45 Usiku wakivutiwa nae.
Ukiwa mtoto unapendwa hakuna mtu ambaye husema mtoto ni mbaya, kila mtoto huonekana mzuri mbele ya macho ya kila mtu, ndicho ambacho kiliwatokea Lulu, Kevin na hata Bow Bow walipendwa kwa utoto wao.
 
NI NGUMU KUKUA NA MASHABIKI
Baada ya zaidi ya miaka 20 tangu kutamba kwake ndani ya filamu za Home Alone leo hii hakuna ambaye anakumbuka kwamba paliwahi kuwepo na binadamu anaitwa Mauclay a.k.a Kevin.
Hata wale walioingalia movie ile hawakumbuki kuhusu Kevin zaidi stori zake zinazosombaa ni zile mbaya zikiwemo za utumiaji wa madawa ya kulevya ambapo mara kadhaa amewahi kukamatwa katika jiji la Oklahoma akiwa na kete za Bangi.
Licha ya kipaji kikubwa alichokionesha lakini ni wazi wengi tulimpenda kutokana na udogo wake, umri wake mdogo ukijumlisha na kipaji chake vikamuongezea umaarufu na mapenzi makubwa kwa mashabiki, leo akiwa naa miaka 36 hakuna anaemtaka tena.
Watu wamemsahau, hawajali kuhusu yeye tena, wamemtema!
Bow Bow alishindwa kuishi katika kilele ambacho kiliwafanya mashabiki wa Hip Hop duniani kuanza kumlinganisha na Lil Wayne.
Skendo zake za mapenzi na kimwana Ciara zikamfanya asahau hata kutunga ngoma za kuwateka mashabiki mwishowe akaona muziki mgumu.
Sasa amejikita kwenye uigizaji, yote haya ni kuonesha jinsi gani ameshindwa kukua na mashabiki.
Wapo wengi ambao waliwahi kutoka katika umri mdogo lakini wameshindwa kuendeleza makali yao, Dogo Janja alitoka katika umri mdogo sana akapendwa na kumteka kila mtu mwishowe akapotea kabisa kabla ya kurudi kwa mara ya pili.
Nani amesahau kuhusu Jaden Smith na Dada yake, Willow walifanikiwa kuteka katika filamu na muziki wakiwa katika umri mdogo lakini sasa wanapambana kurudi, ile huruma ya mashabiki huwa na kikomo pale unapokuwa mtu mzima.
Kinachoangaliwa ni ubora wa kazi, siyo huruma wala mapenzi yale ya utotoni.
 
LULU NAMUACHA KAMA ALIVYO
Mikasa mingi, milima mingi, na vigingi visivyo na ukomo vimezidi kumueka katika Dunia yake mwenyewe tangu alipoibuliwa pale Kaole na Mahsein Awadh ‘ Dk Chein’.
Alipendwa akiwa mdogo na bado anazidi kuwateka/kututeka akiwa katika umri wa kupiga kura, linapokuja suala la kulimea jina lake Lulu hajawahi kuacha nyakati zimpite.
Fikiria skendo na matukio ya kuogofya ambayo amewahi kukutana nayo lakini imani kwa mashabiki wake imeendelea kuwepo pale pale, sijui hata anawapa nini!
April 7, 2012 inawezekana ikawa ya kukumbukwa zaidi kwake kutokana na Gwiji la Filamu, Steven Kanumba kufariki mbele ya macho yake huku akihusishwa na kifo hicho.
Miezi ya kutosha jela kwa mtoto wa aina yake, urembo wake akautumia akiwa Segerea lakini bado ameendelea kukisanua katika ‘industry’ ya Bongo.
Kwanini niache kumueka katika daraja la juu la mastaa waliofaulu katika umri wa utoto hadi utu uzima?
Michael Jackson alitoka angali mtoto na hadi mauti yanamkuta jina lake lilikuwa juu ya mastaa wote duniani, maziko yake yanatajwa kuhudhuriwa na kutazamwa na idadi kubwa ya watu, alitamba utoto hadi ukubwani.
Beyonce Knowles ‘Queen Bee’ katika umri wa miaka 13 tayari alishakuwa staa mkubwa akiwa na kundi lake la Destiny Child, leo akiwa na miaka 35 bado ni staa kama ambavyo alikuwa tangu utoto wake.
Nyuma ya Yvonne Cherly ‘Monalisa’ Lulu anaweza kuwa juu ya wengine wote linapokuja suala la nani ni Muigizaji bora wa Bongo Movie, achana na wale ambao walivamia tasnia  kutokana na uzuri wa sura na maumbo yao.
Pamoja na skendo na matukio yote hayo bado Lulu atabaki kuwepo katika daraja la tofauti na mastaa wengine waliotoka angali wadogo, tutamueka katika kapu moja na Beyonce au Michael Jackson.
Hazitaki zile huruma za utotoni, anataka apendwe kwa ubora wake wa ukubwani.
 

Wiki Hii na Charles James
Kwa maoni 0713 153035

0 Comments: