Saturday, May 20, 2017

Mr Blue ni alama ya mlima uliosimama bila kudondoka


UNAFUNGUA redio unakutana na rekodi ya kibabe ya baki na mimi, unageukia runinga yako unauona wimbo wa mboga saba ambao huwezi kudhani kama msanii aliyeuimba ana miaka 13 kwenye muziki wa Bongo Fleva, pumzi inakushuka tabasamu lazima lijengeke usoni.
Miaka 13 nyuma wakati muziki wa kuimba ukiwa umeanza kushika kasi, mashabiki wanampokea msanii ambaye pengine alitoka akiwa na umri mdogo kuliko waliokuwepo, sura ya kitoto, umbo dogo tena ikisemekana alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza pale Benjamin Mkapa Sekondari,

Kariakoo! ni nani?.
Heri Samir ‘Mr Blue’ alikuwa ameingia katika tasnia ambayo awali watu walikuwa wakiichukulia poa, hakuna ambaye aliuona muziki kama biashara na hata utokaji wake kwa maana ya kurekodi na kutoka kisanii ilikuwa changamoto zisizo na maelezo mazuri ya kusimulia.
Ungeweza kutembea kwa miguu kutoka Temeke mpaka Masaki kwa Master Jay kurekodi au ungewahi mapema kwa P Funk na bado akakuzingua kuingia studio, kwa umri wake angemudu vipi, angeweza kustahimili kwa kipindi kirefu?.
Haikua hivyo tu alitoka katika nyakati ambazo muziki wa Hip Hop ulikuwa katika kilele chake, nani angekusikiliza wewe unaeimba? Waliofanya muziki huo waliitwa wabana pua, mabishoo na majina mengine ya kuudhi, changamoto zilikuwa nyingi nani amesahau ile stori ya ‘kijinga’ kuhusu Blue na Kalapina? Tuachane na hayo, muda umepita!

Kuanzia siku ile aliyoachia wimbo wake wa Blue blue mpaka leo hajawahi kushuka kisanii, hajawahi kupanda pia juu kwa kiwango kikubwa ameendelea kuwepo palepale, kuna wengi aliwakuta kwenye gemu wameshindwa wamekaa pembeni lakini yeye bado yupo.
Wapo waliomkuta yeye tena wakatengeneza majina yao kwa kiwango cha ajabu kumshinda lakini wakakosa muendelezo mzuri ‘consistency’ wakaanguka na mpaka sasa wameshindwa kunyanyuka, yeye bado yupo tena akiachia ngoma kila kukicha zenye ujazo na uwezo wa kutawala redio zote, huo tunauita ufanisi wa hali ya juu!

Kuna utofauti mkubwa kutoka kwa Blue wa Blue blue na kiss kiss na yule wa Tabasamu hadi kwa huyu wa Baki na mimi na Mboga saba, ipo tena sio ndogo, kuanzia muonekano wake mpaka staili ya muziki anaoufanya, twende taratibu!
Jaribu kuwasikiliza wasanii wengi wa Hip Hop staili waliyoanza nayo ya kurap wapo walioanza kuikimbia, msikilize Darasa huyu wa muziki sio yule wa sikati tamaa, Joh Makin wa Hao sio huyu wa Nusu nusu.

Wengi wamelegeza ‘floo’ wapo walioamua kuimba kabisa na kuachana na kurap, Kalapina na ugumu wake alifanya hivyo lakini hali haipo hivyo kwa Blue yeye alitoka kwenye ‘kubana pua’ na kuanza kurap na amewashika mashabiki kwa muda mrefu bila kushuka.
Jaribu kuhudhuria shoo zake utagundua ni moja kati ya wasanii wa muda mrefu ambao wanaweza kumiliki jukwaa kwa muda mrefu bila kuchoka huku akiwarukisha kwata mashabiki kwa namna atakavyo yeye, kwanini ashindwe wakati anaishi mioyoni mwao?.

Atashishindwa vipi ilihali nyimbo alizonazo hazijawahi kuboa nyoyo za wale wanaolipa viingilio vyao kwenda kumtazama? Maonesho makubwa yamekuwa yakitoa majibu kuhusu ubora wake, hakamatiki.

Sio kila msanii anaweza kudumu kwenye huu muziki kwa muda mrefu bila kushuka, pengine Dully Sykes anaweza kushikilia rekodi hiyo kwa sasa lakini Blue ni mmoja wa wale ambao wameutendea haki muziki huu, uwezo wake wa kuachia ngoma zinazoweza kusumbua hadi kwenye bodaboda ndio unaomfanya akubalike kila siku na kuzidi kuwepo hapo alipo kwa muda mrefu.

Kipindi Fulani aliwahi kukabiliwa na skendo za utumiaji wa madawa ya kulevya ‘unga’ sawa! Inawezekana kweli aliwahi kutumia, alikula au alivuta sina uhakika lakini aliwahi kutokeza hadharani na kukiri kwamba alikua akivuta bangi na sigara na sio unga, umejifunza nini hapo?
Uthubutu! Alitambua kuwa tayari kuna kengele ya hatari imegota kichwani mwake, kwamba mashabiki washaanza kumhisi vibaya na alitambua athari ya kuwa na skendo mbaya masikioni mwa mashabiki, angedondoka! Angesahaulika haraka! Angepotea.

Ni nani amewahi kuwa na skendo za utumiaji madawa akabaki salama? Langa? Mungu amlaze mahali pema lakini ‘unga’ ulimuaribia, Chillah je? Sote tunafahamu kiasi gani anapambana kurudia kilele chake.
kwa miaka ya karibuni Chid benz ni mfano ulio hai, kwanini yeye aendelee kuwepo huko? Machale yalimcheza!

Wiki iliyopita nilikuwa niliandika namna ambavyo wakongwe kwenye gemu wanavyopigishwa kwata kwa sababu wameshindwa kumudu kasi ya vijana wa sasa.
Wanaishia kuweka chuki na wivu inayopelekea kuingia shimoni Zaidi, lakini kwa Blue hali siyo hivyo bado ameendelea kuishi kama ‘underground’ na hiyo imezidi kumzidishia heshima yake.

Miezi michache iliyopita ilisemekana aliingia katika mikwaruzano ya kugombea jina yeye na Diamond, eti wote wanajiita Simba lakini nani ambaye angeweza kukaa kimya bila kurushiana maneno na msanii ambaye kwa sasa amelishika soko?

Wengi wanafanya hivyo wakiamini kuwa wanajizidishia umaarufu lakini kwa Blue hali haikua hivyo alitulia kimya na ghafla bifu likaisha, hiyo tunaita busara za mkongwe, yaani kwa hadhi na heshima aliyonayo kwenye muziki ingekua kichekesho kuingia katika ugomvi na ‘dogo’,.


Sio hilo tu hata ugomvi wake na Sugu uliisha vizuri katika masikio ya mashabiki hata kama moyoni wanaendelea nao lakini kutoendeleza chokochoko nayo ilikua heshima kwake.
Blue ni mfano katika gemu ni kisiki kilichoshindwa kukatika kirahisi na bado ameendelea kuotesha mizizi yake, pengine tabasamu ndio rekodi iliyonogesha Zaidi umwamba wake, achilia mbali namna alivyowafanya ‘kitu mbaya’ Dully na Joslin kule kwenye Dhahabu.

0 Comments: