Saturday, May 20, 2017

Diamond, AY wanastahili heshima

KILA unapotaka kuzungumzia mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva katika ngazi ya kimataifa, huwezi kuepuka kutaja majina ya hawa wasanii wawili.
Diamond Platnumz akiwakilisha ngome yake (lebo) ya Wasafi Classic Baby (WCB), huku kipindi cha nyuma AY akiibeba kambi yake ya Unit Entertainment.
Wamekuwa wakipambana sana kuhakikisha muziki huu unafika mbali zaidi na kupata dhamani kubwa kwenye mataifa mengine, na hilo wamefanikiwa kwa asilimia kubwa.
Leo katika safu hii pendwa ëZeze kolaboí, wewe msomaji wangu nakuchambulia jinsi Diamond na AY alivyofanikiwa kupeleka     Bongo Fleva kimataifa kwa kufanya kolabo na wasanii wa nje.
 
Tuanzie Nigeria
Kama kumbukumbu zangu zipo sawa, AY ndiye msanii wa kwanza kutoka kwenye Bongo Fleva kufanya kolabo kubwa na wasanii kutoka Nigeria.
Mwaka 2008 wakati kundi la P Square linafanya vizuri na nyimbo zake kama Temptation na Dome  walikuja Tanzania kufanya ‘show’ , ndipo AY alipoona kuna uwezekana wa kufanyao nao kazi.
Bila kupoteza muda wakaingia studio B Hit’s kwa Prodyuza Hermy B na kutoa wimbo uliokwenda kwa jina ‘Freeze’ ambao ulishangaza wengi na kujiuliza AY amewezaje!
Weka nukta hapo, msanii wa kwanza wa Nigeria kupewa shavu na Diamond ni Davido, ambaye mwaka 2013 kwa pamoja walitoa wimbo uitwao ‘My number one’ uliyomleta Diamond mpya kwenye Bongo Fleva.
Kazi ilifanyika studio za Burn Records kwa prodyuza Shed Clever, licha ya wimbo huu kumtambulisha Diamond kimataifa, pia ulimtambulisha Shed Clever   na kumuwezesha kuwania tuzo ya Afrimma Dalas Texas Marekani.
 
Unapaswa kujua na hili
AY hakuishia kwa P Square tu, bali alikuja kufanya kazi na wasanii kama Goldie Harvey wimbo uliitwa ‘Skibobo’ uliyotoka mwaka 2012.
Goldie Harvey alikuwa mwakilishi wa Nigeria katika shindano la Big Brother Africa (BBA) kwa mwaka 2012, ambapo alianzisha uhusino na msanii wa Kenya Prezzo, kwa mapenzi ya Mwenyenzi Mungu mwaka 2013 alifariki dunia.
Weka nukta hapo, Kama hiyo haitoshi mwaka 2013 AY pamoja na Mwana FA walimpa shavu J Martins kwenye wimbo uitwao ‘Cheza bila kukunja goti’, chini ya prodyuza Marco Chali.
Diamond nae alizidisha mashambulizi kwa kufanya kazi na wasanii kama Iyanya aliyempa shavu kwenye wimbo wa ëBum bumí uliyotoka mwaka 2014. Pia Mr Flavour alichukua nafasi kwa kupewa shavu kwenye wimbo wa Nana uliopikwa na prodyuza Nahreel.
Ili kudhibitisha ubora wake, mwaka mwaka jana amedondosha ngoma aliyowashirikisha P Square, wimbo unaitwa Kidog’, ambao unabamba hadi sasa.
 
Hadi Marekani
Diamond na AY si watu wa mchezo kabisa, wote wawili wanaingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kufanya kazi na wasanii wa Marekani.
AY alianza kwa kumshirikisha miss Trinity kwenye wimbo uitwao Good Look  uliotoka mwaka 2011.
Mwaka 2014 aliachia nyimbo mbili kwa mpingo ambazo alifanya na wasanii wa Marekani.
AY alimshirikisha Sea Kingston kwenye wimbo uitwao Touch me. Pia alimshiriksha tena miss Trinity na Lamiya kwenye wimbo uitwao ëItís going downí.
Video ya wimbo huu ilifanya Marekani, AY anakiri ni moja ya video alizowekeza fedha nyingi zaidi. Tukihamia kwa upande wa Diamond, wimbo aliofanya na msanii wa Marekani ni Marry You ambao amemshirikisha Ne-Y, msanii aliyetamba na nyimbo kama, So Sick na Miss Independent.
Wimbo huo ‘umepikwa’ na prodyuza Shed Clever, na iliwalazimu kusafiri hadi Nairobi Kenya wakati Neyo alipokuwa anafanya ‘show’ huko ili kukamisha kolabo hiyo.
 
Pindi walipokutana
AY alimpa shavu Diamond kwenye remix ya wimbo wa Zigo ambao ulisumbua sana wakati ulipotoka.
AY anasema kama asingempata Diamond katika wimbo huu, basi angemshirikisha msanii Wizkid kutoka Nigeria.Kwa kujiamini AY anasema imefika wakati kwa wasanii wa Tanzania kutengeneza muziki mkubwa bila kushirikisha wasanii wa nje.
Hilo wamefanikiwa kwa asilimia kubwa kwa kuwa tuliona wimbo huu ukifanya vizuri na kuingia katika chati za muziki za vituo vikubwa vya televisheni vya Afrika na Ulaya pia.
Video ya wimbo huu hadi sasa katika mtando wa Youtube umetazamwa na watu zaidi ya milioni 8.8 tangu utoke Januari 22 mwaka jana.
Tumalize hivi, kutambua ukubwa wa hii kolabo AY anawakutanisha maprodyuza watatu ambao ni Nahreel, Marco Chali na Hermy B kunogesha mdundo wake.
Peter Akaro
Kwa maoni 0755 299 596

0 Comments: