Tuesday, July 4, 2017

Nay, Quick Rocka na Saida Karoli, wametaka ganda la ndizi au ubunifu hawana?

MWEZI uliomalizika ambao ulikuwa na siku 30 umekuwa wenye simulizi nyingi za burudani na michezo.
Kiufupi ni mwezi wenye historia yake kama umeufuatilia kwa makini.Tumeshuhudia nchi ya Tanzania ikitembelewa na wachezaji wa mpira akiwemo mchezaji wa zamani wa Uingereza na klabu za Manchester United, David Beckham, beki wa klabu ya Everton na timu ya taifa ya Ufaransa, Schneiderlin pamoja na mchezaji wa Tottenham, Victor Wanyama.

Kwa upande wa burudani tumeshuhudia mengi, kwa mfano uzinduzi wa filamu mpya ya Gabo ‘Kisogo’ aliyomshirikisha Wema Sepetu, filamu hii itaonekana kupitia app, huu ni mwanzo wa mapinduzi katika namna ya kuuza kazi za sanaa kuendana na wakati.

Hapo hapo kwenye buruduni, kwa upande wangu nimekuwa busy sana katika kusikiliza ngoma tatu tu!, ambazo zimetoka mwezi huu. Yakwanza ni Orugambo ya Saida Karoli, Moto ya Nay wa Mitego, na ya tatu ‘Watasema’ ya Quick Rocka na OMG ambayo imetoka jana.

Kwanini Saida Karoli, Nay wa Mitego na OMG
Katika nyimbo hizo tatu nilizotangulia kuzitaja, kama ubahatika kuzisikiliza bila shaka utagundua zimechukua maneno, beat au melody kutoka kwenye wimbo au nyimbo fulani. Kumbuka zote zimetoka mwezi uliomalizika jana (June) wenye siku 30 na masaa 720.

Katika wimbo wa Saida Karoli ‘Orugambo’ ambao video yake ilitoka June 12 mwaka huu, amechukua baadhi ya maneno kutoka kwenye nyimbo tatu tofauti. Amechukua kutoka kwenye wimbo wa Diamond ‘Salome’, amechukua kwa Belle 9 ‘Give It To Me’, na mwisho kutoka kwa Darassa katika ngoma ya Muziki.

Kwa upande wa Nay wa Mitego katika ngoma yake ya Moto, amechukua maneno na malody kutoka kwenye nyimbo tatu, amechukua kutoka kwa Balozi ‘Kwenye Chati’, pia amechukua kwa Juma Nature ‘Hili Game’ pamoja na ngoma ya Mchizi Mox ‘Mambo Vipi’.

Mapokeo yangu ngoma hii ni makubwa kwa upande wa mashabiki wa Nay ambao hupenda yeye anavyowachana watu wazi wazi, tuachane na hilo.

Tukiangalia ngoma ya OMG ‘Watasema’ ambayo wamemshirikisha Quick Rocka ambaye ni kama boss wao, ngoma yao imechukua chorus kutoka kwenye wimbo wa TID a.k.a Mzee Kigogo ‘Watasema Sana’ iliyotoka zaidi ya miaka 10 nyuma. Well done, wote wamenifurahisha kwa ngoma zao.

Binafsi nimekuwa nikijiuliza nini maana ya mfululizo wa nyimbo za aina, naomba nisinukuliwe vibaya, sijapiga, ila nyimbo za aina hii zinatoa picha ya aina gani katika muziki wetu?. Muziki umekua, wasanii wanatafuta uwepesi au wasanii wameishiwa ubunifu. Yote yanaweza kuwa majibu.

Saida Karoli ni msanii wa siku nyingi na ukubwa wa jina lake unaheshimika zaidi miaka 15 sasa, kuchukua baadhi ya vitu kutoka kwenye nyimbo za Belle 9, Diamond na Darassa ambao pia walichukua nao kutoa kwenye wimbo wake wa Maria Salome ni sawa kwa sababu anatafuta kujenga ushiwishi kwa wanunuzi wa bidhaa yake kwa sasa ambao wengi ni vijana.

Ni wazi wimbo huu umependwa kutokana na nyimbo hizo tatu kufanya vizuri, hivyo Saida Karoli amepata wepesi katika mapokeo ya wimbo huo. Je huu uwepesi ulikuwa akiutafuta au umekuja kwa bahati mbaya?, ni vigumu kusadiki hilo kwa sasa, hivyo naomba tuachane nalo.

Nay wa Mitego na ngoma za Mchizi Mox, Balozi na Juma Nature, je anatafuta ushawishi katika kizazi cha sasa au kilichomtangulia (old school)?, kama ni sasa mbona Nay anafahamika na kazi nyingi ambazo hadi zinapendwa na viongozi wakubwa serikalini, kama ni kwa upande wa old school njia aliyotumia nina mashaka nayo.

Kizazi hicho hakiwezi kumkubali kwa kurudia kile ambacho wameshakifanya, hivyo hapa Mr Nay angetakiwa kuwa mbunifu kwa kuleta kitu kipya ambacho kingekuwa na nguvu ya ushawishi kwa pande zote mbili.

OMG ni miongoni mwa makundi machache yanayofanya vizuri kwa sasa katika muziki wa hip hop Bongo, wanaonekana watafika mbali. Binafsi sikuona sababu ya wao kuchukua chorus ya TID kwa namna walivyofanya vizuri na wimbo wao 'Uongo Na Umbeya', katika wimbo wao verse ya kila mmoja ni kali, kwenye flow kama kawaida yao huwajawahi kuniangusha, ila chorus!

Quick Rocka ameitendea haki chorus, ameonyesha uwezo wake wote na kweli kitu kimetoka kikali sana, ila kulikuwa na ulazima gani kuchukua chorus ya wimbo mwingine. Sitaki kuamini OMG na Quick Rocka walishindwa kuandika chorus, pengine hawakutaka kuwa wabunifu zaidi kwenye hili, walichukulia poa, walizembea, yote pia yaweza kuwa majibu, ila niwapongeze kwa kazi nzuri waliyofanya.

Binafsi naunga mkono wasanii kuazimana vionjo katika nyimbo zao ila basi kuwe na makubaliano yatakayonuisha pande zote mbili kwa sababu baada ya OMG kutoa wimbo huo TID alikuja juu na kudai fidia ya Sh milioni 40 kutokana na wao kutumia wimbo wake bila makubaliano lakini hadi hadi sasa wameshafikia muhafaka.
Je huku ni muziki kukua, wasanii wanataka wepesi au wasanii hawataki kuwa wabunifu?.
Kwa Maoni 0755 299596

0 Comments: