ZIPO nyakati ukirudisha kumbukumbu nyuma na kuangalia wapi Tanzania imetoka katika tasnia ya filamu na muziki unaweza kutikisa kichwa kwa uchungu au kwa furaha. Vyote vinawezekana.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000 hakuna ambaye alisikiliza muziki wa Nigeria hakuna msanii wa Nigeria aliyekuwa staa hapa kwetu kumshinda Juma Nature, Profesa Jay, Lady Jide wala Mr Paul.
Zaidi wenye kupenda muziki walisikiliza ngoma kutoka Marekani kwa wakali waliokuwa wakitamba kama Sean Paul, Jay Z, Madonna, Shaggy na R Kelly. Sentensi rahisi Nigeria hawakua na maajabu ya muziki.
Lakini ni wazi katika upande wa pili wa Sanaa kwa maana ya filamu walikuwa wapo mbali sana, hatukuwa daraja moja nao, walituacha maili nyingi na kila kitu walichofanya kilikuwa kigeni kwetu.
Wakati ambao Desmond Elliot, Mama G, Omotola Jalade, Ramsey Noah na Emeka Ike wakiwa wasanii maarufu na kanda za filamu zao zikiuzwa kwa wingi katika maduka yetu Kariakoo, sisi bado tulikuwa bize tukiangaika na tamthilia zetu za saa tatu usiku, Jumamosi, Jumapili na Jumatatu.
Tulikuwa nyuma maili 10 ya walipokuwa wenzetu, haikushangaza pale filamu zao za kichawi zilipotufanya tujenge imani ya kwamba Wanaigeria ni wachawi kuliko watu wote Afrika (inawezekana ikawa kweli ).
Aina ya filamu zao za kichawi ikatufanya hata sisi kuiga stori na staili zao, ushahidi upo katika filamu ya Nsyuka, Safari na Takadini.
TOA NIGERIA, WEKA BONGO MOVIE
Mapambano ya wasanii wa filamu mwanzoni yalikuwa makubwa, watu waliumiza vichwa kuhakikisha wanatoka kuigiza michezo ya kwenye TV na kuja kuteka na kuzipoteza kabisa filamu za Nigeria.
Tukumbuke kabla ya hapo muziki wa Bongo Fleva ulishateka rasmi mashabiki, wasanii wao walikuwa mastaa wakubwa ndani na nje ya Nchi, wakasumbua kwenye Media zote.
Wapo waliofanikiwa na kujenga maisha yao, wapo waliopata umaarufu ukawalevya na kujikuta wakidumbukia shimoni, wapo waliomiliki wanawake wazuri, nyumba na magari ya gharama.
Muziki ulikuwa mali kushinda Filamu.
Girlfriend ikawa filamu ya kwanza kufanya mapinduzi ya sanaa ya maigizo nchini, hatimaye taratibu watu wakaanza kujaribu kufanya kile kilichowapa umaarufu akina Genevieve Nnaji nchini kwetu.
Ray na Kanumba kwa ushirikiano wa Game 1st Quality wakatushtua na filamu kali ya Johari ile hatujakaa sawa wakatuchapa na Sikitiko la Moyo, mwisho filamu zikaiteka Bongo.
Kila mtu akanogewa na filamu zetu za ndani na kuanza kusahau kuhusu ‘movie za kichawi’ za Kinigeria, Ray, Kanumba, Johari na Mainda wakaiteka Bongo na stori kuhusu Ramsey Noah, Jim Iyke ikaanza kupotea taratibu.
Bongo movie ikaota mizizi, kwa ubora wa kazi zao ikamea vichwani mwetu.
FILAMU ZIKAIKABA KOO MUZIKI
Pamoja na kwamba muziki ulianza kukiki mapema kabla ya filamu lakini ni wazi baada ya Kanumba na ‘nduguye’ Ray kuamua kuwekeza kwenye filamu walifanikiwa kugeuza vichwa vya mashabiki ambao walianza kununua kazi zao huku wakiwapa utayari ‘tention’ kulinganisha na muziki.
Filamu zikateka kila kona na hata wasanii wake wakapata umaarufu mkubwa kuliko ule waliokuwa nao Bongo fleva, nani amesahau namna ambavyo ziara ya Kanumba, Ray, Johari na Irene Uwoya kule Rwanda na DR Congo walipokuwa wakitamba na filamu yao ya Oprah?
Mapokezi waliyoyapata katika ziara hizo yalionesha namna gani filamu inapiga hatua nje ya Nchi, maandamano ya pikipiki, magari na miguu yaliyofanywa na watu wakati walipoenda kuwapokea uwanja wa Ndege yalikuwa mageni kwetu.
Filamu ilitikisa Bongo bwana! Hakuna ambaye hakutaka kumtazama Kanumba, kila mmoja alitamani kusikia Ray angekuja na kali gani, alipotoka JB na swahiba wake Richie Richie kila mtu aliangaika kupata nakala ya CD zao.
Kabla ya kifo cha Kanumba hakuna ambaye aliangaika kusema filamu za Nje zifungiwe mara zizuiwe sijui kodi na lugha nyingine zisizoeleweka, ubora wa kazi ulikuwepo, mashabiki walizitamani filamu za nyumbani.
Ni ukweli mtupu kabla ya kifo cha Uncle JJ Bongo Movie ilitamba kuliko Bongo Fleva, kama ni ngumi muziki ulikuwa umepigwa TKO.
BONGO MOVIE IPO ‘ICU’
Nilicheka kwa dharau niliposikia eti Bongo Movie wanaandama wakiongozwa na ‘fulani’ eti kushinikiza Serikali izuie filamu za nje kuingia nchini eti kwa sababu kodi za movie za nje hazikatwi kama za kwao.
Eti lengo likiwa ni kuwataka Watanzania kusapoti filamu zao na siyo za nje, huku ni kuishiwa kwa mawazo yakinifu kwa watu wanaounda tasnia hiyo.
Hivi hii ndio Bongo Movie ambayo ilipiganiwa na watu zaidi ya miaka 20 nyuma? Bongo Movie ile iliyofanikiwa kuteka filamu za Nigeria kabla ya kuzifurumishia mbali?
Bongo Movie ile ambayo iliwafanya Ray, Uwoya na Kanumba kupata mapokezi ya kifalme Congo, Rwanda na Burundi kuwashinda marais wa Nchi hizo?
Aibu kubwa sana aibu ambayo mwili wa Steven Kanumba uliolala pale Kinondoni unaweza kutikisika.
Yaani kwa uzembe wao wenyewe wameharibu Soko la filamu zao wenyewe na sasa wanataka huruma ya mashabik!
Hivi JB huyu wa sasa ni yule aliyecheza Swahiba na Regina? Stori tamu zinazosisimua zimeenda wapi? Ray bado unajiita The Greatest? Kama jibu ndio tafadhali liondoe hilo jina.
Hakuna ubunifu katika filamu za siku hizi, kila siku mastaa ni wale wale, Dada zetu warembo ndio wanaocheza katika nafasi nzuri kila filamu, nyumba na magari wanayotumia hayabadiliki.
Haishangazi kuona hivi sasa wamekimbilia Muziki na kutoka kimapenzi na Wabongo Fleva, haishangazi siku hizi wanatumika kisiasa, hainishangazi pia kuona siku hizi mashabiki wanapenda kufuatilia Instagram akaunti ya Uwoya, Wolper, Ray kuliko kuuliza filamu zao mpya zinatoka lini.
Aibu yetu aibu yao wenyewe! Hivi Wema Sepetu bado unaigiza?
Mwandishi : Charles James
0 Comments:
Post a Comment