Tuesday, August 1, 2017

Mungu afuta machozi ya Happiness Magese

HATIMAYE safari yenye mateso na maumivu ya kila aina kwa mwanadada mrembo baada ya kushinda taji la Miss Tanzania mwaka 2001 Happiness Magese,inaonekana kufika mwisho baada ya Mungu kusikia kilio chake kwa kujifungua mtoto wa kiume anaitwa Prince Kairo Michael Magese..

Mateso na maumivu yaliyotokana na ugonjwa wa muda mrefu uliokuwa unamsumbua Happiness Magese unafahamika kwa jina la endometriosis.Ni ugonjwa uliokuwa unamsababisha maumivu makali pindi anapokuwa kwenye hedhi.

Kwa waliopata nafasi ya kumsikia Happiness akielezea mateso ya ugonjwa huo waliokuwa wanatokwa na machozi.Ameteseka sana na katika kutafuta unafuu amefanyiwa operesheni mara 13.Yote hiyo akijaribu kuondoa maumivu ambayo yamemtesa kwa zaidi ya miaka 26.

Ikafika mahali akapoteza matumaini ya kuitwa mama kwani ugonjwa huo ulielezwa kuwa umeharibu mfumo mzima wa uzazi.Happiness hakuwa mwenye furaha kwani mbali ya kusumbuliwa na maumivu alitamani kuitwa mama lakini akaona ni kama vile kwake haitawezekana.

Siku zote alielezea namna ambavyo anatamani siku moja aitwe mama.Miaka ikawa inakatika bila mafanikio, muda mwingi akawa anatembea na dawa za kutuliza maumivu na inapobidi operesheni.
Ameishi maisha ya mteso lakini siku zote alimiani Mungu ipo siku atasikiliza kilio chake.Kilio kikubwa ilikuwa ni lini atapata mtoto kwani wakati wote hakuwa na raha ya maisha kutokana na ugonjwa uliokuwa unamsumbua.

Hakuficha kwa Watanzania na hata kuilezea dunia kwa ujumla  namna anavyoishi kwa mateso.Anafedha, ana mali lakini kwake haikuwa kitu zaidi ya kufikia siku moja awe mama.
Jitihada za madaktari kwa nyakati tofafuti walimshauri ili aondokane na maumivu ni vema akaondolewa kizazi.Kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye hakuwa tayari kuondoa kizazi,  hivyo alikubali kuwa anafanyiwa operesheni kadri madaktari walivyoona inafaa.

Mungu ni mwema na sasa ndoto za Happiness zimekuwa kweli.Anaitwa mama baada ya kujifungua mtoto wa kiume.Baada ya kujifungua mtoto huyo aliamua kuandika ujumbe mrefu wa kumshukuru Mungu kwa kumpatia mtoto na anataka awe baraka.

Happiness akatumia ukarasa wake wa Instagram kumtaka mwanaye kuwa
baraka, matumaini na muujiza kwa mamilioni ya wanawake duniani wanaotamani kupata watoto lakini wameshindwa kutokana na kuwa na ugonjwa huo.

Sehemu ya maelezo yake ameandika “Ukalete matumaini, imani na miujiza kwa mamilioni ya wanawake duniani wanaotamani kubeba watoto wao kama nilivyokuwa nikitamani kukubeba wewe.
“Ukue na kuibadili dunia kwa ajili ya wengine. Ukamuamini Mungu na kumiliki miujiza yake,”ameandika mrembo huyo huku akielezea safari yake ya mateso ambayo ameishi nayo mwili kwa muda mrefu.Ikafika mahali anajikojolea bila kujitambua.

Binafsi nilipata nafasi ya kukutana na Happiness na kumsikiliza , ukweli nilikuwa natokwa machozi kila nilipokutana naye.Hongera Happiness maana naamini mateso yako yamefika mwisho.
Sasa anaitwa mama, kilio chake kimesikika lakini kikubwa zaidi Happiness anakuwa nembo nyingine inayothibitisha uwezo wa Mungu kwenye kutenda miujiza kwa wenye kukata tamaa.

Kuhusu ugonjwa wake Happiness ametumia gharama kubwa ya fedha kutafuta matibabu lakini haikuwezekana.Safari ya maumivu na mateso hatimaye Mungu anamfuta machozi kwa kumpa mtoto wa kiume.

0 Comments: