Tuesday, July 4, 2017

‘Couple’ ya Jux na Vanessa inaponikumbusha ya Beckham na Victoria

“KWENYE kila yalipo mafanikio ya Mwanaume nyuma yake yupo Mwanamke shupavu aliyefanikisha hayo,” itoshe kusema hivyo.
Msemo huu umekuwa ukitumika katika mahusiano ya kimapenzi na haswa pale mwanaume ambaye kabla ya mahusiano yake alikuwa na maisha ya kawaida lakini baada ya kuanza mahusiano na msichana fulani mambo yake huzidi kumnyookea.

Ni jambo linalotia hamasa sana pale unapopata mwenza anaeweza kukushauri na kukutia moyo katika kile unachokifanya kiasi cha kupiga hatua zaidi ya ulivyokuwa kabla ya kukutana nae.
Katika jambo kubwa ambalo nimejifunza ni kwamba wanaume wengi ambao wamekuwa na mafanikio ya kawaida wanapojiingiza kwenye mahusiano na wanawake ambao tayari wameshafanikiwa basi hujikuta wanapiga hatua kubwa zaidi ya wanawake wao endapo watakuwa kweli na hasira ya mafanikio.

Imewahi kutokea kwa mastaa wengi wa muziki, filamu hadi Soka ambao walikuwa na majina ya kawaida lakini ghafla walipoanzisha mahusiano na mastaa wa kike walifanikiwa zaidi ya walivyokuwa awali.
 
Jux na Vanessa
Wakati Jux anatoka na wimbo wake wa Napata raha miaka takribani mitano nyuma hakuna ambaye alionekana kuwa na presha nae, wengi walimuona ni msanii mzuri lakini hakuepo aliyekiri na kulikuza jina lake.

Tukumbuke kuwa Jux alianza kusikika kimuziki kabla hata ya ujio wa Vanessa lakini hakuna ambaye alikuwa na 'shobo' nae, wengi waliishia kumsifia kuwa msanii ambaye anajua kupangilia zaidi mavazi na wala sio uwezo wake kisanii. Kuingia kwa kasi kwa Vee kwenye Muziki wa Bongo Fleva kuliwafanya hata wasanii wa kike waliokuwepo kuamka ili kutoboa zaidi kimataifa.

Baada ya penzi lake na mrembo Jack Cliff kuingia mdudu kutokana na kimwana huyo kushikiliwa nchini China, ndipo penzi lake na Vee lilipoanza kuibuka na kushika kasi kwa spidi ya 4G.
Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba hadi wanaanza mahusiano yao, bado Jux alikuwa akionekana ni msanii wa kawaida mbele ya Vee, dada alikuwa ameshauteka muziki kuanzia Bongo hadi nje, Jux alionekana kama mwanafunzi kwa Vee.

JUX anapiga hatua zaidi ya Vee
Ule msemo wa kwamba popote yalipo mafanikio ya mwanaume kuna mwanamke nyuma unaonekana katika ëcoupleí hii ya Jux na Vee, kimsingi ukiangalia tangu wameanza mahusiano yao utakubaliana na mimi kwamba kijana anapiga hatua zaidi kulinganisha na yule binti.
Mahusiano yao ndio ambayo yamemfanya Jux azidi kuimarika zaidi kisanii huku akiongeza zaidi ‘fanbase’ baada ya Vee kumkutanisha na Kundi la Weusi (Joh Makin, G Nako na Nikki wa Pili ) hivyo kujikuta 'akiiba' pia mashabiki wa Hip Hop kutoka kwa kundi hilo.

La kukumbukwa hapa ni kwamba mwanzoni Jux alikuwa akionekana kama ëbishooí Fulani lakini kitendo cha kuwa kampani moja na Weusi sasa kimewafanya hata wale mashabiki wa Hip Hop kuamini jamaa ni mwenzao, hii maana yake ni nini?

Kwamba hivi sasa anaeza kufanya shoo Arusha ambapo ndio Weusi wanatokea na kupata mashabiki kama anafanya kwenye mkoa wake wa nyumbani, na kukumbusha pia Vee kwao ni Arusha hivyo Jux anajiona yupo ukweni.

Ninasema kuwa Jux anapiga hatua zaidi ya Vee kwa sababu ukiangalia hatua zake za kisanii utaona zimesogea zaidi ya ëdemuí wake ambaye hakuna mabadiliko yoyote ambayo yameongezeka kwake kwani tangu anatoka jina lake limeendelea kuwa pale pale, halishuki wala kukua.

Kwanini nawafananisha na Beckham, Victoria?
Wakati  Mwanasoka, David Beckham jina lake likianza kuchomoza kwenye ulingo wa Soka katikati ya miaka ya 90 katika klabu ya Manchester United ghafla akajikwaa katika penzi la Mwanamuziki, Victoria Posh kutoka kundi maarufu nchini Uingereza la Spice Girls.

Wakati wanaanza penzi lao mwaka 1997, Becks alikuwa mtu wa kawaida sana lakini alivoanzisha mahusiano na Posh, jina lake likakua kwa kasi ya ajabu, kuanzia uwanjani hadi nje ya ulingo wa Soka ambapo alipata tenda kibao za matangazo yaliyomfanya kuwa miongoni mwa wanamichezo matajiri duniani.

Leo hii ukiangalia mafanikio binafsi kati yao utaona jinsi gani Becks kamzidi mke wake maili nyingi, kuanzia mafanikio ya kiuchumi hadi kujulikana, ni wachache sana hivi sasa utawauliza kama wanamjua Posh wajibu ndio, lakini hebu uliza wanaomjua Becks utaona balaa lake.

Lakini siyo Becks tu na Jux ambao majina yao yamekuzwa na mahusiano yao, nani ambaye atabisha hapa kuwa Diamond Platnumz ustaa wake uliratibiwa zaidi na penzi lake na Wema Sepetu?
Kipindi Diamond anatoka jina na mafanikio yake yalikuwa ya kawaida sana mbele ya Wema lakini baada ya mahusiano yao nafikiri wote tunaweza kusema nani kafanikiwa zaidi hivi sasa.

Si wao tu hata Chris Brown penzi lake kwa Rihanna ndilo ambalo limemfanya leo kuwa maarufu na kupata mafanikio makubwa zaidi.
Juzi Harmonize kakiri kwamba wakati anaanza mahusiano na Jackline Wolper hakua na gari na Wolper alikuwa amemuacha mbali sana kimafanikio, lakini jaribu kuwafuatilia baada ya miaka mitatu. Yale yale ya Jux na Vee, Becks na Posh.
Kwa maoni 0713 153035

0 Comments: