Saturday, June 24, 2017

Bongo Movie tuonesheni kuwa Kanumba hajaondoka na filamu zake

GHAFLA sana nimeikumbuka ile Jumamosi ya April 7, 2012, ndio siku aliyokata kauli muigizaji nguli ambaye alishaanza kuisogeza tasnia ya filamu nje ya mipaka ya Tanzania tena akiwa ameshafanya kazi na wanaigeria wenye heshima zao akiwemo Ramsey Noah na Mercy Johnson! Steven Kanumba.

Ghafla pia nakumbuka kwamba leo ndio mkesha wa mwaka mpya na 2016 haitojirudia tena, ni mwaka ambao Bongo Fleva imezidi kupasua mawimbi na kupenya kila mahali, heshima za kutosha kwa Diamond, Soka pia lilijitutumua heshima kwake Mbwana Samatta sina haja ya kurudia alichokifanya.

Ghafla nakumbuka kuna kitu kinaitwa Bongo Movie, ndio! Bongo Movie ile ambayo miaka sita nyuma ilikuwa maarufu haswa tena kila kijana akiwa na ndoto za uigizaji na wala siyo kuimba, katika kuwaza kwangu nikakumbuka Lulu na Richie, Mei mwaka huu walitwaa tuzo katika ule usiku wa Tuzo kule Lagos, Nigeria.

Lakini je tuzo zile zilikuwa na maana kwao? Ziliongeza kitu kwenye tasnia? Zilibadilisha mitazamo ya wasanii kwa kiasi gani? Maswali mepesi lakini magumu kujibika, twende pamoja!
Wenzao wa Bongo Fleva ndani ya kipindi cha miaka miwili wamepiga hatua kubwa sana, wameshiriki tuzo nyingi tena kila wasanii wengi wakipata nafasi hiyo achilia mbali kwamba Diamond ndio alifungua njia ya kushiriki tuzo kubwa za MTV na BET, leo kuna Vanessa, Navy Kezno, Ali Kiba na Joh Makin, hiyo tunaita kuthubutu!

Fikiria tangu kufariki kwa Kanumba hakuna mafanikio yoyote ya maana ambayo Bongo Movie inaweza kusimama hadharani na kujisifu nayo, kumbuka mpaka anakwenda kulala katika ile nyumba yake ya futi sita alikuwa ameshafanya kazi na Noah mmoja kati ya mastaa wa filamu ambao hawana mfano wake Afrika.

Baada ya kuondoka yeye ni nani aliyethubutu kufunga safari kwenda Nigeria kutengeneza filamu, ni nani amesafiri hadi Hollywood kutafuta fursa za kushirikiana na akina Tony Cruz, Will Smith na Jennifer Lopez?
Kipindi Fulani ilisemekana Wema Sepetu yupo kwenye mawasiliano na ‘lover boy’ wa Ghana, Van Vicker lakini siku hazijaganda zimekimbia na mwishoe tumegundua kuwa ile ilikuwa danganya toto wala hakuna kazi yoyote waliyofanya, vijana wa Instagram wanaita kiki.

Unataka kuamini kuwa Kanumba kaondoka na Bongo Movie yake? Hebu jiulize kwa upole wako wapi wasanii ambao walitamba katika filamu zake? Oke! lugha nyepesi ni kwamba wapo wapi wasanii ambao aliwatoa yeye? Tuulizane bila hasira tu kisha tupeane majibu watu wa filamu.

Kuna wale watoto alicheza nao kwenye This is It na Uncle JJ (Jeniffer na Patrick) walionekana wakali sana, walitisha pengine hawakua na kipaji ila kwa sababu walifanya na Kanumba wakaonekana mafundi leo hawapo na sijui kama wanaweza kuwa na stori tamu midomoni mwa mashabiki tena.

Kama ulidhani ni wale watoto tu unajidanganya, kuna kundi kubwa la wasanii walitolewa na Stevie lakini wameshindwa kuishi ndani ya filamu wakasepa, yupo wapi Shaz Sandry King’asti wa nguvu aliyekuwepo kwenye ile the Shock?
Patcho Mwamba kaamua awe mtangazaji, Ben hayupo kama zamani, Mayassa nilimsikia ameamua kuwa mpambaji wa waigizaji (make up) kwaa sababu hapati dili za kucheza filamu kama ilivyokuwa enzi ya The Great.

Ukifuatilia hata afya ya kazi za wasanii wengine ambao walikuwa wakichuana nae hivi sasa ni kama imepungua, fikiria ni nani atashituka tena akisikia Ray katoa filamu mpya, JB amebaki jina kila siku filamu zake ni zilezile lazima awe mtu wa kupiga makelele.
Hemed amebaki kuwa yuleyule kwa miaka mingi na hakuna la ziada lililoongezeka kwake, Mlela ameamua kukimbilia Kenya kucheza tamthilia hapo utapata picha hali ipoje, kuna mtu anaitwa Gabo anafanya vizuri na pengine anafuata nyayo (nitakuja kumuongelea siku nyingine).

Unataka kujua ni kwa kiasi gani kifo cha Kanumba kimeiathiri Mongo Movie? Jaribu kutazama ni filamu ngapi ambazo Wema atacheza kwa mwaka? Irene Uwoya je? Aunt Ezekiel vipi? Ndio kwanza wapo bize na wasanii wa muziki wakibanjuka nao wamesahau tasnia yao na wala hawajali.

Diamond alipovuka mipaka na kufanya remix ya Number One na Davido kila mtu aliyatamani mafanikio yake, na toka pale tumeshuhudia kolabo za kutosha baina ya wasanii wetu na wa nje, tena zingine wakituomba wao, lakini kwenye filamu haijawa hivyo kila siku wanajipanga kila kukicha wanasema muda haujafika, ni aibu kwa kweli! Aibu kwa Ray, JB, Wema na kiwanda cha filamu kwa ujumla.

Leo hakuna mtoto ambaye anatamani kuwa staa wa filamu kwa sababu amekosekana mtu wa kuwavutia huko ‘mentor’ kila mmoja anataka kukimbilia kwenye muziki kwa sababu wanavutiwa na Diamond, Ali Kiba na Vanessa.

Wakigeuka kwenye filamu hakuna jipya na majibu yake wanayo dada zetu, Snura na Shilole waliamua kukimbia kabisa na kuanza kuimba, yule Wema ameamua kuwekeza katika muziki anamiliki wasanii wake kwenye kampuni yake ya Endless Fame.

Sanaa ni fani ambayo kama wasanii wetu wakiamua kuitumia vizuri wangefika mbali sana, lakini hakuna mabadiliko yoyote kwenye filamu, wakongwe wameendelea kusimama palepale walipokuwepo.

Damu changa nazo hazileti changamoto kwa veteran matokeo yake tunauanza mwaka wa tano tukiwa na kumbukumbu za Kanumba kuondoka na filamu zake huku Ray akiwa bize kutengeneza ‘Six packs’ na kulinda penzi lake na King’asti Chuchu Hans.
Kwa maoni 0713 153035
Wiki Hii na Charles James

0 Comments: