Rais na mwanzilishi wa asasi ya Mabalozi wa Utamaduni wa Mwafrika (African Culltural Embassy Association) Bwana Colpas Numfor kutoka nchini Cameroon (Katikati) akionesha nyaraka mbalimbali za usajili wa asasi yake wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya BASATA ya Jukwaa la Sanaa. Kushoto kwake ni Katibu wa chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli na Kaimu Mkurugenzi wa asasi hiyo nchini Tanzania Bw. Maganiko Charles
Na Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wameiomba Serikali kumalizia ujenzi wa ukumbi wa Sanaa za maonesho unaojengwa kwa zaidi ya miaka minane sasa makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) eneo la Ilala sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa ya Baraza hilo mapema
wiki hii, wasanii hao walieleza kwamba kwa sasa kuna ufinyu wa kumbi za za
maonesho hali ambayo imekuwa ikiwafanya wasanii hao kukosa maeneo ya kufanya
sanaa zao hivyo kumalizika kwa ukumbi huo itakuwa ni ahueni kubwa kwao.
“Ukumbi huu ni
muhimu sana kwetu, wengi tuliutazama kama mwanzo wa ufufuaji wa Sanaa za
majukwaani lakini sasa ni muda mrefu hauoneshi dalili za kumalizika. Kuna kila
sababu ya ukumbi huu kukamilika ili kutusaidia katika maonesho yetu” alisema
Msanii Khalid Kambau.
Kwa upande
wake msanii wa Sanaa za maigizo Christian Kauzeni ambaye pia ni mwenyekiti wa
chama cha wasanii waigizaji mkoani Dar es Salaam alisema kwamba kutokana na
ukumbi huo kutazamwa kama mkombozi wa wasanii kuna kila sababu ya kuangalia
mbinu mbalimbali ili kuhakikisha unakamilika mapema iwezekanavyo.
Awali
akiwasilisha mada kwenye Jukwaa hilo la Sanaa iliyohusu ‘Ubora wa Filamu na Changamoto zake’
msanii na mzalishaji filamu maarufu nchini William Mtitu alisema kwamba tasnia
ya filamu chini imepata umaarufu na kukua ingawa bado changamoto za uharamia,
elimu na masoko zimeendelea kuiathiri.
“Kwa sasa
filamu zinazozalishwa zimekuwa na ubora kuliko huko nyuma. Tatizo liko kwenye
elimu kwa wasanii, uharamia na masoko. Kulikuwa na maduka zaidi ya sabini na
tano yanayouza kazi za wasanii wa filamu lakini kwa sasa yamebaki sita tu.
Wengi wameamua kuuza kazi za nje mbazo ni nafuu. Hii ni hatari” alisisitiza
Mtitu.
Aliongeza
kwamba pamoja na Serikali kuirasimisha sekta ya filamu bado kuna changamoto ya
kazi zinazotoka nje kutokuwekewa stempu za mamlaka ya mapato huku kukiwa na
uharamia unaotishia bei za filamu halali zenye stempu hizo.
Jukwaa la BASATA
limekuwa likifanyika kwa mwezi mara mbili siku za Jumatatu na wiki hii kulikuwa
pia na utambulisho wa asasi ya ubalozi wa Utamaduni wa Mwafrika ambayo
imeasisiwa nchini Cameroon, Afrika Magharibi mwaka 2014.
Mdau wa
Sanaa na utamduni Bw. Francis Kaswahili naye alitoa mchango wake kwenye
Jukwaa la Sanaa. Alitoa wito kwa wasanii kuhakikisha wanakuwa na kauli
moja katika kuhakikisha wanasimamia maslahi yao.
Afisa Masoko kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Pastory John
akitoa maelezo mbalimbali kuhusu urasimishaji wa sekta ya filamu nchini
kwenye Jukwaa hilo la Sanaa. Msanii na mzalishaji filamu nchini William Mtitu (Kulia) akiongea na wadau wa Sanaa (hawako pichani) wakati akiwasilisha mada iliyohusu ‘Ubora katika filamu na changamoto zake’ kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kushoto ni Katibu wa chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli.






0 Comments:
Post a Comment