Monday, April 9, 2012

Kifo chake chahisiwa kuwa cha utata

Seth bosco, kaka wa kanumba
Mama yake na Kanumba, Flore Mtegoa

“AMKA Kanumba, mama amekuja. Amka baba. Unameremeta baba, ndoa yako ya mwisho hii, kwaheri mwanangu”

Hayo ni maneno aliyokuwa akiyatoa mama yake mzazi marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitokea Bukoba.

Katikati ya kilio-huku akichanganya lugha ya kisukuma- mama huyu alielezea jinsi alivyopata taarifa za msiba,adhuhuri ya Aprili 7.

Blanketi la huzuni lilifunika anga la makazi ya msanii huyu mara baada ya mama yake Kanumba kuwasili na kusababisha baadhi ya waombelezaji kupoteza fahamu.


Mdogo wa marehemu akiri ni kifo cha utata

Seth anaitaja kauli ya mwisho kuisikia katika kinywa cha Kanumba ilikuwa ni ‘Nisubiri’.

Anasema, jioni ya tarehe 6 April, marehemu alimwambia Seth kuwa angependa watoke kwenda matembezini pamoja.

“Ilipofika mida ya saa sita za usiku, nilimwambia kuwa, mimi nimekwishajiandaa, akasema ‘nisubiri’ na kisha akaingia chumbani mwake” alisimulia Seth.

Alisema: “Kanumba akiwa chumbani kwake, aliingia binti mmoja, ambaye ninamfahamu kuwa ni mtu wake wa karibu, kwa kuwa namfahamu, sikushangazwa na ujio wake, na aliingia chumbani kwa Kanumba”

Seth alisimulia zaidi na kusema, bada ya muda alisikia sauti zilizoonyesha mgogoro wa aina fulani toka chumbani humo na alipotaka kuingia, mlango ulifungwa kwa funguo.

“Nilisikia kauli ya Kanumba ikimwambia Lulu (Elizabeth Michael) ambaye pia ni msanii mwenzake “Yaani unapigiwa simu na mwanaume wako mbele yangu” na baada ya dakika kadhaa za mzozo chumbani, Lulu alitoka akisema kuwa Kanumba ameanguka” alisema Seth.

“Kama alisukumwa ukutani, basi lazima jeraha lingeonekana katika ubongo, lakini ripoti inaonyesha hana jeraha, na mimi nilimkuta marehemu akiwa anatokwa na povu mdomoni, macho yamemtoka, huku akikoroma, cha ajabu hakutokwa damu” alisema.

Aliongeza: “Hata hivyo, bado tunasubiri uchunguzi zaidi wa polisi”

Pamoja na kuwa katikati ya majonzi mazito, dada wa marehemu Kabela Kajumulo alisema, hana maneno ya kuweza kumchanganua mdogo wake.

“Ninachoweza kusema ni kuwa, tumepata pengo lisiloweza kuzibika” alisema

Wasanii wa filamu na muziki walikuwa wakishughulika au kujadili hili na lile katika msiba huu mzito. Miongoni mwao ni msaniii na rafiki wa karibu wa marehemu Kanumba, Blandina Chagula(Johari)


Msanii Wema Sepetu akiongea na vyombo vya Habari kuhusiana na kifo cha Kanumba
Baadhi ya wasanii mbalimbali walikuwepo katika mazishi ya msanii Kanumba
Umati wa watu waliokuwepo msibani

Johari: nimepata pigo

Chagula alidokeza uhusiano wake na marehemu na kusema, Kanumba ni zaidi ya rafiki kwake, kwani hawakujuana katika maigizo tu, bali walicheza pamoja tangu utotoni.

“Nimesoma na Kanumba Mwanza, shule ya msingi Bugoyi, lakini si hivyo tu, bali mama yake Kanumba na mama yangu ni marafiki wa karibu” anasema Chagula.

Anaongeza: “Tulikutana tena hapa jijini, lakini yeye akisoma shule ya Jitegemee mimi, shule nyingine, ndipo tulipojiunga katika maigizo katika kikundi cha Kaole,”

Chagula anasema, amepata pigo kwa kuondokewa na Kanumba kwani alikuwa ni zaidi ya kaka na zaidi ya rafiki. Anaongeza kuwa, Kanumba alikuwa ni mshauri na alimuonya pale alipokosea.

Chagula anayataja mambo matatu ambayo angependa wasanii wengine wamuige Kanumba kuwa ni uchapa kazi, kujihifadhi na ustaarabu.

“Hana mfano wake, ni mstaarabu, ana upendo na anajiheshimu,” anasema Chagula.

Wasanii wamsifu Kanumba kwa kujihehimu

Ruth Suka, (Mainda) ni miongoni mwa watu waliowahi kufanya kazi na marehemu Kanumba na alimtaja kuwa ni miongoni mwa watu wachapa kazi na wanaojiheshimu.

Suka alisema, Kanumba alikuwa ni kijana mstaarabu na kabla hajawa maarufu, alikuwa akiogopa mno kuwa karibu na wanawake.

“Ni mtu aliyejisitiri mno na mambo yake, lakini mazingira yake ya usanii yalimfanya aanze kuchangamka na kujichanganya na watu wa rika zote. Kwa kifupi ni mtu wa kanisa” alisema Suka.

Emanuel Myamba ni msanii aliyesoma shule ya Jitegemee pamoja na marehemu Kanumba, alimzungumzia na kusema, marehemu hakuwahi kunificha kuhusu mahusiano yake.

“Alipokuwa na mahusiano na Wema nilijua, hata mahusiano yake na Nargis Mohamed nayo niliyafahamu, lakini hizi habari za Lulu nilikuwa sizifahamu,” alisema Myamba

Aliongeza kuwa,Kanumba alikuwa ni mtu aliyejiheshimu … pengine hakutaka kuweka wazi mahusiano yake na Lulu kutokana na tabia za msanii huyo.

“Lakini sikuwahi kuhisi kama atatembea na binti yule” alisema Myamba.

Rais aahirisha safari kuhudhuria msiba

Rais Jakaya M Kikwete jana alifika katika msiba wa msanii huyu, na alionyesha kusikitishwa na kifo hicho kiasi cha kusitisha safari yake ya nje ya nchi.

“Nimeguswa na msiba huu, na nilikuwa nisafiri lakini nimeamua kuja hapa kuwapa pole ndugu na wasanii wote,” alisema Rais.

Ujumbe wake mzito na wa mwisho katika blogu

Aprili, 6 Kanumba alitoa ujumbe ulioonekana kutabiri kifo chake, akiyanukuu maneno ya Mwanafalsafa, Albert Pine, yaliyosema:

“Tunachofanya kwa ajili yetu tunakufa nacho. Lakini tunachofanya kwa wengine na kwa ulimwengu, kinadumu na ni cha milele”

Kanumba, alizaliwa Agosti 12, 1984. Amesoma shule ya msingi Bugoyi iliyopo Shinyanga. Elimu ya sekondari ameipata katika shule mbili tofauti, Bugoyi Sekondari Shinyanga, na Dar es Salaam Christian Seminary.

Mwaka 2004 alijiunga na shule ya Sekondari ya Jitegemee kwa elimu ya kidato cha tano na sita.

Kanumba alileta mapinduzi ya filamu Tanzania, kwa kazi yake ya kwanza kabisa ya ‘Johari njia Panda’.

Hadi sasa amecheza filamu zaidi ya 40, ndani na nje ya nchi, huku filamu yake iliyokuwa mbioni kuingia sokoni mwezi huu ikiwa ni ‘Ndoa Yangu’

Kanumba anatarajiwa kuzikwa jijini Dar es Salaam, siku ya Jumanne, Aprili 10, katika makaburi ya Sinza. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

0 Comments: