Tuesday, January 17, 2012

MZEE JANGALA AKUNWA NA JUKWAA LA SANAA

Sehemu ya wadau waliohudhuria katika Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala.
Mdau wa Sanaa akitaka ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali yahusuyo Sanaa za majukwaani.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idaya ya Ukuzaji Sanaa, Bi. Shalua akifafanua jambo wakati akihitimisha mjadala kuhusu Sanaa za majukwaani kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kushoto ni Mzee Jangala na Kaimu Mratibu wa Jukwaa la Sanaa, Aristide Kwizela.
Msanii Nguli wa sanaa za maonesho, Bakari Kassim Mbelemba (Mzee Jangala) aikizungumza na wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linaloendeshwa na BASATA kila siku ya jumatatu.Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya ukuzaji sanaa, BASATA Vivian Shalua


Na: Mwandishi wetu

Msanii nguli wa Sanaa za Maonesho, Bakari Kassim Mbelemba (Mzee Jangala) amesema kuwa programu ya Jukwaa la Sanaa inayoendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni chuo tosha kwa wasanii katika kuwapa elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali ya sekta ya Sanaa.

Akizungumza wiki hii, kwenye programu hiyo katika ukumbi wa BASATA, Ilala Sharif Shamba, Jangala alisema kuwa, Jukwaa la Sanaa ni jambo la kujivunia na ni chachu ya kukua kwa Sanaa.
“Jukwaa la Sanaa ni programu inayonifanya nithubutu kusema, sasa Sanaa ni kazi, maana kazi yoyote ili ifanywe kwa ufanisi inahitaji elimu, uratibu na mwongozo, hivyo wasanii tuitumie fursa hii adimu” Jangala alisema.

Aliongeza kuwa, programu hii imekuwa ikiwaleta wataalam na wadau mbalimbali wenye uzoefu katika sekta ya Sanaa hivyo, kwa wasanii ambao wamekuwa wakihudhuria toka mwanzo wamepata mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kukuza na kuendeleza vipaji vyao.

Alisisitiza kuwa, Sanaa inabadilika na kumezwa na teknolojia mpya zinazokuwa zinajitokeza hivyo, ni lazima wasanii wajenge utamaduni wa kutafuta maarifa mapya na kuwa wabunifu huku wakizingatia maadili ya kitanzania.

Kuhusu wasanii kulewa umaarufu na sifa, alishauri kuwa ni vema wakabadilika na kufanya kazi zao kwa bidii na ubunifu zaidi kwani, sifa ya msanii inakuja yenyewe kutokana na kazi anazozalisha na kupeleka kwa jamii inayomzunguka.

“Sifa ya mpishi hutolewa na mlaji, kwa hiyo wasanii wanapotengeneza kazi zao wasijisifu wenyewe bali wasubili kusifiwa na msikilizaji au mtazamaji” alishauri Mzee Jangala.

Alizungumzia pia suala la wasanii kutegemea vipaji tu pasipo kuingia darasani na kusema kuwa hilo haliwezi kukuza sekta ya sanaa na badala yake tutakuwa na kazi zinazoandaliwa kwa msukumo wa soko na si taaluma ya Sanaa

“Wasanii ni lazima watambue kuwa, mbolea ya kipaji chochote kile ni elimu. Ni vigumu sana kutegemea kipaji tu pasipo kukipalilia kwa taaluma ya sanaa husika”

Kwa upande wake, kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa, Vivian Nsao Shalua alishauri wasanii kulitumia Jukwaa la Sanaa ili kuzijua sheria, taratibu na mbinu mbalimbali zitakazo waongoza katika shughuli zao za Sanaa.

0 Comments: