Friday, January 27, 2012

BASATA NA JESHI LA POLISI KUENDESHA PROGRAMU MAALUM YA SANAA SHIRIKISHI


27/01/2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

BASATA NA JESHI LA POLISI KUENDESHA PROGRAMU MAALUM YA SANAA SHIRIKISHI KATIKA KUFANIKISHA POLISI JAMII TAREHE 30/01/2012

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania limeandaa programu maalumu ya Polisi Jamii na Sanaa Shirikishi itakayofanyika Jumatatu ya Tarehe 30/01/2012 kwa lengo la kuwaelimisha wasanii, wadau wa sanaa na jamii kwa ujumla kuhusu dhana ya ulinzi shirikishi kupitia Sanaa.

Programu hiyo inatarajiwa kufanyika makao makuu ya BASATA yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam ambapo lengo kuu ni kutoa fursa kwa wasaniii, wadau wa Sanaa na wananchi kwa ujumla kujifunza na kuona umuhimu wa matumizi ya Sanaa shirikishi katika kujenga dhana ya ulinzi shirikishi inayoratibiwa na kusimamiwa na Jeshi la Polisi Tanzania.

Aidha, programu hii, inalenga kutoa elimu kwa wasanii na wadau wa Sanaa juu ya mbinu mbalimbali za kutumia Sanaa katika kupambana na vitendo vya kihalifu ili kujenga jamii yenye amani na utulivu.

Ikumbukwe kuwa, BASATA kila Jumatatu limekuwa likiendesha Programu ya Jukwaa la Sanaa ambayo imekuwa ikitumika kama chanzo mahsusi cha habari na elimu kwa wasanii na wadau wa Sanaa. Programu hii ya Polisi Jamii na Sanaa Shirikishi itatumia Jukwaa hili katika kuifikia jamii.

Katika programu hii, vitengo mbalimbali vya Jeshi la Polisi kama Uhamiaji, zima moto, usalama barabarani, udhibiti madawa ya kulevya nk. vinatarajia kushiriki ambapo mbali ya kupambwa na burudani kutoka jeshi hilo itakuwa na kipindi cha maswali na majibu ambapo changamoto na kero mbalimbali kuhusu usalama wa raia zitatolewa ufafanuzi.

Ili kuonesha jinsi sanaa shirikishi ilivyoweza kuleta mabadiliko kwenye dhana ya polisi jamii nchini, Kundi la Sanaa la Lumumba Theatre la jijini Dar es Salaam nalo linatarajia kutoa burudani kemukemu ambazo zitabeba elimu juu ya Sanaa Shirikishi na Polisi Jamii.

Baraza linatoa wito kwa Wasanii na wadau wote wa Sanaa kujitokeza kwa wingi kwenye programu hiyo ili kujifunza mbinu mbalimbali za kufikisha ujumbe kupitia sanaa na hata kuitumia Sanaa katika kujenga jamii yenye utulivu.

Sanaa ni Kazi, kwa pamoja Tuikuze na Kuithamini

Godfrey Lebejo - KATIBU MTENDAJI (K)

0 Comments: