Friday, October 1, 2010

DR REMMY AMPONGEZA SHAKIRA

Dr.Remmy
MWANAMUZIKI mkongwe wa nchini Dk Remmy Ongala amemwagia sifa mwimbaji na mtunzi mahiri wa muziki wa taraabu nchini Shakila Saidi kwamba ni msanii mwenye uwezo mkubwa katika muziki huo.

Akizungumza na burudanikilasiku nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es salaam alisema kwamba Shakila ni mwimbaji na mtunzi ambaye anastahili sifa kutokana na umahiri wake katika muziki huo.

Dk Remmy alisema kwamba Shakila amekuwa akitunga tungo ambazo hazichuji tokea alipoanza kujuhusisha na muziki huo na pia tungo zake zina ujumbe kwa jamii.

"Shakila ni msanii wa kweli katika muziki wa taarabu,tokea mimi namsikia mpaka leo hachuji kabisa ni vema tumpongeze kwa kuwa na kipaji"alisema Dk Remmy.

Mwanamuziki huyo ambaye kwa sasa ameokoka,alisema Shakila ameonyesha heshima katika muziki wa taarabu nchini kutokana na tungo zake kuwa na heshima kitu ambacho wasanii wengi wa sasa wa muziki huo wanakikosa.

"Unaweza kwenda katika maonyesho Shakila akiwa anaimba ukafurahi sana ,kwani tungo zake zina ujumbe mzuri tu na usiopitwa" alisema Dk Remmy.

Dk Remmy alisema pamoja na kuwa kwa sasa ameokoka,ila hali hiyo haimnyimi haki ya kueleza umma hisia zake kuhusu muziki wa aina yoyote kutokana na uzoefu wake walionao katika muziki.

"Kwa kweli nimeamua kumpongeza Shakila kwani tungo zake,sauti yake kweli ni nzuri na yeye ni mkombozi kwa muziki wa taarabu hapa nchini" alisema mwanamuziki huyo.

Shakila ni mmoja wa waimbaji wakongwe wa kike hapa nchini katika muziki wa taraabu ambapo alinza kuimba tokea akiwa na umri mdogo katika kundi la Luck Star lilokuwa na maskani yake jijini Tanga.

Akiwa na kundi hilo aliweza kushiriki vema katika kuendeleza muziki wa taraabu nchini kiasi cha kumpatia umaarufu mkubwa nchini.

Alijiunga na kundi la JKT taraabu mwaka 1984 ambapo yupo mpaka sasa akishiriki kutunga na kuimba tungo ambazo zimetokea kupata umaarufu mkubwa kila kona.

Aidha alisema kutokana na hali hiyo ameamua kumpongeza mwanamama huyo ambaye kwa sasa anafanya kazi yake ya sanaa ndani ya kundi la JKT Taraabu jijini Dar es salaam.

Source:Na James Nindi

0 Comments: