MAKALA

King Kiba anapozidi kutuonesha unyonge wake kwenye video
Charles James
 NASHUKURU Mungu nilikuwepo zama ambazo mashairi na sauti nzuri ndivyo vilivyohusudiwa zaidi kwenye muziki wa Bongo Fleva, nyakati ambazo kama ulikuwa na uwezo mdogo wa kuimba usingerekodi kwa P Funk na Master Jay.

Labda hujanielewa hapa nazungumzia zile enzi biashara ya muziki ilitegemea zaidi usikivu wa masikio ya shabiki, wakati ambao Audio zilitamba, yaani zama ambazo muziki mzuri ni ule uliotamba kwenye Radio na wala siyo ule uliofikisha ‘viewers’ wengi You Tube. Twende taratibu.
Kama ilivyotokea miaka ya 1760 wakati Dunia ikishuhudia mapinduzi makubwa ya viwanda nchini Uingereza na Ulaya ndivyo ambavyo hata kwetu hivi sasa tumeshuhudia mapinduzi ya Muziki, ndiyo! mapinduzi ambayo wapo wanaopinga na wengine wakiyafurahia.

Baada ya kushuhudia enzi za muziki mzuri ni ule unaoyafikia na kuyaburudisha masikio ya shabiki, nimepata bahati ya kuziona zama mpya za muziki wetu zama ambazo kila kitu kimebadilika, kuanzia uandishi, midundo hadi staili ya muziki.

Katika mabadiliko haya ya muziki ndipo ambapo soko la muziki linaonekana kuingiliwa na kirusi cha video, huwezi kufanikiwa kwenye muziki hivi sasa kama uwekezaji wako kwenye video ni wa kinyonge.
Kama soko limehamia kwenye mtandao wa You Tube hivi sasa nani ambaye ataisikiliza sauti tamu ya Rama Dee au muziki mzuri ulioshiba wa Steve R&B na kuacha kuitazama video kali ya Kijuso ya Queen Darleen na Rayvanny, mapinduzi ya muziki yametubadilisha.
 
MAPINDUZI YA MUZIKI
Tangu muziki ubadilike na kuonekana ni biashara ambayo inaweza kuingiza fedha nyingi na kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana kuishinda hata Wizara ya Maliasili na Utalii, kila mmoja ameamini katika sanaa, vijana wamehamisha akili na nguvu zao huko, wanahitaji Sanaa, wanaamini katika Muziki.

Mapinduzi haya ndio ambayo yametufanya leo tushuhudie wasanii wengi wakipiga ‘mtonyo’ mwingi kwenye kazi zao kutokana na kubadilika kutoka kufanya muziki kwa ajili ya kuelimisha na kuburudisha sasa umehama na kuwa biashara, biashara ambayo inawafanya vijana wailipe Serikali kodi nyingi, Muziki unalipa!

Huwezi kufananisha muziki aliofanya Profesa Jay miaka 16 nyuma na hiki ambacho Joh Makin na Bill Nas wanakifanya, iko hivi Juma Nature ufalme wake aliujenga kwa kupenya kwenye masikio ya mashabiki, akafanikiwa kutuaminisha kwa kile tulichokisikia kwake, masikio yetu yakageuka kuwa mateka.

Mtaje msanii ambaye amefanikiwa katika muziki wetu kwa sasa, hapa sihitaji U-team, ni wazi Diamond amefanikiwa sana katika muziki wetu.
Siyo Bongo, Kenya wala Uganda ambapo ni mashemeji zake, Nigeria kaiweka mikononi mwake, Afrika Kusini inakiri ufalme wake na sasa kaimaliza Afrika anakaribia kuiteka Dunia, kwanini kafanikiwa?

Jibu ni jepesi sana Diamond kafanikiwa kuhama na mabadiliko yaliyoletwa na Mapinduzi ya muziki mapinduzi ambayo hayakuhitaji Sime, Panga wala mtutu wa Bunduki kuyakamilsha tofauti na yale ya Januari 12 kule Zanzibar.
Jamaa kafanikiwa kuhama na muziki anafanya kile ambacho kinawezekana kwa wakati sahihi, anapambana kuhakikisha muda haumuachi, ni rahisi kujiuliza kabla ya ufalme wake si alikuwepo mtu mbona hivi sasa hatambi? 

Kwa hiyo inampasasa kukaza buti haswa, suala la mapinduzi ya muziki yeye ni mmoja kati ya watu wanaofaidika nalo, kwamba video zinathaminiwa hivi sasa kushinda audio, ukitaka kuamini hili rejea kauli ya Ommy Dimpoz kwamba wapo wanaonunua ‘viewers’ youtube.
 
KING KIBA MAPINDUZI YAMEMPITA?
Inawezekana nafasi yake iliyokuwepo miaka sita nyuma siyo hii aliyonayo leo, nani angeleta miguu yake kushindana nae wakati Mapenzi yanarun Dunia ikiwa inapigwa kwenye spika zako?
Achana na MacMuga, Njiwa hadi Cinderella sogea hadi kwenye Ya Karim, sauti na utunzi vilikwenda shule yule kijana aliyetoka na Nenda Kamwambie angesubiri sana, Kiba alikamalika aliuteka muziki haswa.

Baada ya kupumzika na kurejea kwa kishindo kwenye gemu na rekodi mubashara ya Mwana wengi wakauona ufalme wa Kiba ukirudi mikononi mwake, lakini kumbe akasahau miaka mitatu aliyopumzika muziki yalitokea Mapinduzi ya Muziki.
Mapinduzi ambayo yaliifanya Sauti yake kwenye Mwana ionekane ya kawaida mbele ya video ya wimbo wake huo, wengi wakaponda ubovu wa kichupa na mwishoe akatoa utetezi kwamba Director, GodFather alimfanyia hujuma. 

Zitafute video za wimbo wake uone kama kuna maajabu kwenye kazi zake hizo, weka pembeni Nagharamia aliyofanya na fundi Christian Bella hebu tukumbushane biashara nzuri ya video aliyowahi kuifanya Ali? Jibu ni hakuna.

Kila anapotoa amekuwa anakosea anashindwa kufahamu zile zama za ufalme wa sauti na utunzi zimepitwa na yale mapinduzi ya muziki yametuathiri, hivi Ali hujui kwamba kiungo kinachopima muziki mzuri siku hizi ni Macho na siyo Sikio? Ngoja tuzungumze.

Nimeitazama video ya Aje remix tena na tena nikarudia kuitazama kwa mara nyingi nafsi yangu imejiridhisha kwamba video Ile ni mbovu na haina hadhi ya ‘ufalme’ alionao Ali Kiba.

Achilia mbali kutudanganya na sauti ya M.I ilihali hayupo kwenye kichupa kile bado siyo video inayoweza kumfanya shabiki akubali kuunguza nyama jikoni ili tu akaione video ya Aje remix, kwanini umekubali kuwa mnyonge wa biashara ya video?
inawezekana ukapata ‘viewers’ wa kutosha youtube lakini isikupe kiburi kwamba ni kwa sababu ya ubora wa video hapana ni umwamba wa jina lako ndio unaowafanya watu wamalize bando kukuangalia, lakini tambua unawanyima cha kuzungumza mashabiki wako mbele ya team ya yule yamaa anaetamba na Marry you.
Kwa maoni 0713 153035



0 Comments: