SPORTS

Enrique kung’atuka Barca

KOCHA wa Barcelona, Luis Enrique ameeleza kuwa huwenda akaachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Tangu Barca ikumbane na kipigo cha mabao 4-0 mbele ya PSG katika mchezo wa ligi ya Mabingwa barani ulaya, presha ya kufukuzwa imekuwa ikimkabili Kocha huyo ambaye ameiwezesha Barca kutwaa vikombe viwili vya La Liga tangu aanze kuinoa na kimoja cha Ligi ya mabingwa.

“ Hakuna presha yoyote inayonikabili kutoka kwa uongozi juu ya mustakabali wa kibarua change, nachoweza kusema mahusiano yangu na uongozi ni mazuri pamoja na wachezaji kwa ujumla, Barca ni familia yangu, lakini naweza kuondoka mwishoni mwa msimu ili nipumzike.
Tayari majina kadhaa ya makocha wanaoweza kumrithi kocha huyo yameweza kutajwa ambapo Kocha wa Sevilla, Jorge Sampaoli akipigiwa chapuo, wengine wanaotajwa ni Jurgen Klopp wa Liverpool na Kocha wa zamani wa PSG, Laurent Blanc.

Yanga yarejea katika mbio za ubingwa

KLABU ya Soka ya Yanga imerejea kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuwachapa Maafande wa Ruvu Shooting mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ambao walifungwa mabao 2-1 kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya mahasimu wao wa Simba, walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kuandika bao lake la kwanza dakika ya 33 kwa mkwaju wa penati uliopigwa na winga wake, Simon Msuva.Penalti hiyo ilitokana na beki wa Ruvu, Mayoka kuunawa mpira uliopigwa na mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa ndani ya eneo la hatari.
Dakika ya 45 ya mchezo Chirwa alioneshwa kadi nyekundu baada ya kuupiga mpira chini na hivyo kutafsriwa kama dharau kutokana na mwamuzi kuwa amepuliza kipyenga kuashiria kuna madhambi yametendeka.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini ni Yanga ambao waliendelea kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa na ndipo walipofanikiwa kuandika bao la pili kupitia kwa mshambuliaji aliyeingia akitokea benchi, Martin Emmanuel aliyeunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Msuva.
Kwa matokeo hayo Yanga inazidi kuisogelea Simba baada ya kufikisha pointi 52, wakiwa nyuma ya vinara hao wa Ligi Kuu kwa pointi mbili huku wote wakiwa wamecheza michezo 23 na hivyo kubakiza michezo saba kumalizika kwa Ligi hiyo.




NG’olo Kante amebeba mafanikio, kilio kwa Chelsea na Leceister 


Charles James
SIMULIZI ya kusisimua kama siyo ya kushangaza kuhusu kiungo wa Cheslea, NG’olo Kante ni kwamba wakati anawasili katika ofisi za Kocha wa Leceister City, Claudio Ranier zilizopo katika uwanja wa King Power kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kusajiliwa, mmoja wa maofisa alimzuia kuingia ndani.

Ofisa yule alimzuia kuingia akidhani Kante alikuwa kijana wa shule na siyo mchezaji aliyekuwa amekuja kwa ajili ya kusajiliwa.
Kimo cha futi tano inawezekana kilimlevya ofisa huyo bila kujua alikuwa anazungumza na mchezaji anaekuja kuwapa ubingwa wa Ligi kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Leceister.
Wanasema usimdharau wala kugombana na usiyemjua leo heshima waliyoipata Leceister msimu uliopita ilitokea miguuni kwake, Mashabiki wanajua na hata yule ofisa aliyemzuia pale King Power anafahamu na kukiri hilo. Weka pini hapo!

Baada ya kuwasha moto akiwa na Caen ya Ufaransa aliyojiunga nayo 2013 na kuisaidia kuipandisha Ligi kuu ya Ufaransa kisha, ubabe wake katika eneo la kiungo ndiyo uliomfanya Ranieri kutamani kuwa na mchezaji wa aina hiyo kwenye timu yake.
Baada ya Kocha Nigel Pearson kunusurika kushuka nayo daraja msimu wa 2014/15, Leceister waliamua kumtimua na kumpa timu Ranieri ambaye wengi walimtazama kama Kocha asiyekuwa na bahati ya ubingwa wa Ligi.

Na alipotua yeye akawaza kusajili wachezaji ambaoa anamini watamsaidia kumaliza nafasi nzuri kwenye Ligi, nikukumbushe tena watakaomsaidia kumaliza nafasi nzuri siyo kutwaa ubingwa.
Timu yenye uwanja unaobeba mashabiki 32,000 huku ikiwa haina hata mashabiki katika mabara mengine inawezaje kutwaa ubingwa mbele ya matajiri wa Manchester United, City, Chelsea au Arsenal?

Siyo Ranieri wala wachezaji wake akiwemo Kante walifahamu ubingwa unatua kwao, na hata walipokuwa wakikaribia kutwaa ubingwa huo ilionekana kama ndoto, maajabu na historia kama ambavyo Blackburn ilifanya hivyo mwaka 1995.
Achana na magoli 41 ambayo kwa pamoja Ryad Mahrez na Jamie Vardy walifunga, sahau kuhusu Nahodha, Wes Morgan alivyoongoza jeshi lake ndani ya uwanja, nyuma ya mafanikio ya Leceister alikuwepo yule ‘mbilikimo’ aliyezuiwa getini na yule ofisa akidhaniwa kuwa mwanafunzi, NG’olo Kante.

Uwezo wake wa kupora mipira na kugawa kwa haraka kwenye pembe za uwanja ndio kulimfanya Mahrez aone kazi ya kupiga pasi za mwisho kwa Vardy ilikuwa nyepesi kuliko Ozil kumpigia Sanchez.
Takwimu kwenye Ligi ya Ufaransa zilimtaja kama mchezaji aliyepora na kuingilia mipira mara nyingi zaidi msimu wa 2014/15 na msimu uliopita akiwa na Leceister aliongoza tena pale kwenye ardhi ya Malkia akipora mpira mara 175 na kuingilia mara 157.

Siyo Matic, Emre Can wala Cocquelin aliyesimama juu yake, aliifanya kazi ya pacha mwenzake Danny Drinkwater kuona mpira ndio kazi nyepesi kufanya duniani, ni ukweli usiofichika kwamba mafanikio yao yalianzia na kumalizikia katika miguu ya Kante.

Baada ya kuwa na msimu waa jasho, machozi na damu kabla ya furaha kuja mwishoni,sasa ikaja ofa ya maana mikononi mwa wachezaji wengi mastaa wa leceister, Mahrez na Vardy walihitajika Arsenal wakati Kante aliliwa na Antonio Conte aliekuwa amekuja kuichukua Chelsea.

Wakati wenzake wale wawili wakiamua kuiendeleza heshima yao pale King Powe, Kante yeye aliwaza tofauti aliamini kuwa kiwango chake siyo saizi ya Leceister tena, unaanzaje kukataa kujiunga na Chelsea sehemu ambayo utapata mshahara mnono, utakua na uhakika wa ubingwa na kujenga zaidi jina lako?

Tangu ameondoka Leceister imekua siyo ile iliyotoa vipigo kwa wakubwa msimu uliopita, wamechoka na sasa wapo nafasi ya 17 wakijaribu kuukimbia mstari wa kushuka daraja, hali yao ni mbaya na haionekani kama watabaki Ligi kuu msimu ujao, pengine wakapishana na Newcastle.
Jaribu kuangalia maisha yake pale kwenye daraja la Stanford, Kante amegeuka kuwa muhimili wa kikosi cha Conte kama alivyomrahisishia kazi Drinkwater kule King Powe ndivyo anavyomfanya Matic aufurahie mpira.

Katika kila eneo ulipo mpira jezi namba saba anayovaa Kante utaiona, anapora mipira na kuzima mashambulizi ya wapinzani lakini kwa spidi hiyo hiyo ataanzisha ‘move’ ya timu yake.
Hazard anakufurahisha namna anavyopasua kutoka pembeni mwa uwanja kuingi katikati, Costa anafunga mno, ile safu ngumu ya ulinzi ya Chelsea ‘Catenaccio’ inamfanya Conte awe na uhakika wa kutofungwa lakini wote hao wanafanya kazi zao kutokana na ubora alionao Kante.

Chelsea wanacheka kwa sababu ya Kante anawapa vitu vingi uwanjani ni kiungo aliyekamilika uwanjani, anaifanya timu nzima ijione ipo sehemu salama.
Ni sawa na nyumba yenye wanawaka wengi na mtoto mmoja wa kiume, hata kama ni mdogo wanawake wale watajiona salama kwa sababu wana mwanaume ndani.

Mafanikio ya Chelsea msimu huu ni mbinu za Conte hakuna anaebisha lakini chemsha kichwa chako kuwaza maisha yao bila Kante msimu yangekuaje? Jiulize ujipe jibu mwenyewe.
Leceister City zaidi ya Kante hakuna mchezaji mwingine mkubwa aliyeondoka, Mahrez, Vardy, Drinkwater, Morgan na Gray wote wapo, shida ipo wapi? Wamechoka? Tukubaliane timu iliundwa kupitia yeye sasa ameondoka Ranieri hajui afanyaje.

Mafanikio ya Chelsea yapo kwenye miguu ya Kante, leo mashabiki wanacheka na kutembea kifua mbele kwa sababu yake, kilio kisichokwisha pale King Power pia kilianza baada ya ‘jeshi’ hili kuamua kuondoka! Faida huku hasara kule, Soka!

0 Comments: